Kwa ufupi kunakuwa hakuna ubora wa harusi au mwenendo mzima unakuwa hauko vizuri.
Kuna familia ambazo wanajitahidi kupanga vizuri na kufanya sherehe vizuri na kuna nyingine zinaboronga na kuacha watu wakijiuliza tatizo lilikuwa nini?
Vitu vya kuzingatia kutokana na mtizamo wangu ni kama ifuatavyo:
Maharusi mnatakiwa kuandaa mpango wa sherehe mapema kabla ya ndugu na watu wengine kuwaandalia
Kuna watu wanashtuka kuhusu hili ila ninachotaka ujue ni kwamba sherehe ni ya kwenu ninyi maharusi mambo yanapokwenda vizuri hiyo ni kumbukumbu ambayo mtabakinayo maisha yenu yote na ikienda vibaya kumbukumbu hiyo ni ya kwenu ninyi hao ndugu na jamaa watakuwa nyumbani kwao na ninyi kwenu. Hivyo basi ninyi ndio mpango wenyewe na hivyo mnatakiwa kuiandaa sherehe yenu na namna mnavyotaka ionekane kabla ya mtu mwingine yeyote ili kumbukumbu yenu isiharibiwe na mambo kufanyika kama kawaida.
Unatakiwa kujua watoa huduma wote, na ubora wa kazi zao. Kumekuwa na tabia ya wanakamati au ndugu kuamua MC gani ashereheshe harusi yako, mpiga picha na video wamtafute wao, mapambo watafute wao n.k. Ukweli wa mambo ni kwamba ukikosea kwenye MC hata kama mpiga picha za video ni mzuri kiasi gani hautaipenda video yako, hivyo basi ushauri wangu ni kwamba maharusi mtafute MC mapema ambaye ana kitu mnachotaka, nyimbo mnazotaka kwa mpangilio mnaouhitaji. Mtafute mpiga picha mzuri mwenye viwango mnavyohitaji na mpambaji atakayekidhi mahitaji yenu.
Katika kusema hivyo, epuka kumbi ambazo wanalazimisha mapambo ni ya kwao na chakula ni kwao. Hapo kuna uwezekano mkubwa kupata kitu ambacho hamkihitaji sana. Ingawa kuna kumbi ambazo wako makini kwenye eneo hilo ila bei zao ni za juu.
Jitahidi kwenye kamati yako kuwa watu wenye maamuzi yako na mapendekezo yako. Hapa ni umuhimu wa kuwa na marafiki wa kweli ambao watahakikisha waende kulingana na matakwa yako. Hapa uwe makini kwani kuna watu wanataka kuvuna kwenye harusi yako kwa kushawishi MC wanayemjua, mpambaji wanayemjua na hata mpishi wanayemjua ili wapate cha juu. Usishangae kwa nini wanang’ang’ania fulani ndio anaweza na huduma yake nzuri. Fanya utafiti mapema zaidi hata kabla vikao havijaanza kama miezi sita hadi miezi minne kabla ya harusi yako.
Ndugu ni wasumbufu sana hata kuliko unavyofikiri. Hapa ndugu wataniwia radhi, ingawa kuna familia ambazo ndugu zake ni wastaarabu na hutaka ndugu yao mambo yaende vizuri lakini wengine hawana msaada kabisa usumbufu wao utauona kwenye michango wakati wa sherehe na wanataka kuhudhuria hata kama hawajachangia chochote. Kwa ufupi usiweke imani yako kubwa kwao, wanaweza kukuangusha na ukajikuta umefanya sherehe ukiwa na msongo wa mawazo.
Hakikisha sherehe yako inaendwa kwa muda. Kitu ambacho kinachosha kwenye sherehe nyingi ni kuwa na mambo mengi yasiyo na msingi na kuishia kupoteza muda, ndio maana watu wengi huja karibu na wakati wa chakula ili ale atoe zawadi kama anayo aondoke. Ukiwa mwenye akili hakikisha MC wako anatumia masaa matatu hadi manne, hutaamini watu watakavyosimulia sherehe yako ukijipanga vizuri kwenye muda na mtiririko wa matukio.
Andaa Fungate yako vizuri. Haiwezekani ufanye harusi watu wale na kunywa haafu unaenda fungate siku tatu, hapo utakuwa hujajitendea haki. Wakati wa fungate ni kupumzika na kumjua kwa ukaribu zaidi huyo mkeo na yeye kukujua. Huu si wakati wa kwenda kusalimia wakwe, hapana huu ni wakati wa ninyi wawili kuwa peke yenu ikiwezekana mbali kabisa na sehemu ambayo watu wanawafahamu mpaka mtakapo rudi kutoka huko.
Mambo hayo yote pokea ushauri ila usiache ndugu au mtu yeyote akuharibie sherehe yako kisa unamheshimu unaacha anaboronga. Kumbuka hiyo ni kumbukumbu yako ya maisha yenu ya ndoa. Watu wengi wameumizwa sana na kuachwa na majeraha ndani ya mioyo yao, lakini una uwezo wa kuyaepuka au kupunguza. Be smart.
No comments:
Post a Comment