Social Icons

Pages

Thursday, May 26, 2016

MAMBO 10 UNAYOTAKIWA KUYAJUA KUHUSU MCHUMBA WAKO KABLA HAMJAOANA


Unadhani kuwa unajua kila kitu kuhusu mume wa maisha yako? Mahusiano mengi hukoma kwa sababu ya masuala ya mawasiliano, uongo au shakhsia zisizoendana. Mengine hufikia kikomo kwa sababu wanandoa hawakuchukua muda kujuana.
Famasia yako ya Ndoa Maridhawa imekuletea mambo 10 ambayo unatakiwa kuyajua kuhusu mwanaume wa maisha yako kabla hujachukua hatua zaidi. Iwapo unayajua baadhi, basi endelea kufuatilia zaidi na zaidi:
1. MALENGO YA KWELI YA KAZI YAKE
Huwenda unaijua kazi yake… lakini unajua kuhusu kazi ya ndoto yake? Unajuaje iwapo atabadili kazi yake baada ya miaka 5? Tambua mapema iwapo mumeo anataka kuwa meneja, kibarua au mkurugenzi wa kampuni au shirika. Anaweza akawa na wazo la kumiliki biashara zake mwenyewe.

2. RADIAMALI YAKE (reaction):
Mzee wangu mmoja aliwahi kuniambia: “Unaweza kujua kuhusu mtu fulani kwa kutazama namna anavyoshughulikia mambo”. Kauli hii inatufundisha kujua kuhusu ghadhabu, hasira na subira ya mtu husika. Hili linaweza kukuonesha namna mtu huyo alivyo. Kupitia radiamali ya mtu ndipo unapoweza kujua silka yake. Lizingatie hilo.

3.   ENEO ANALOPENDA ZAIDI DUNIANI
Tambua eneo analolipenda zaidi katika maisha yake, na ambalo humpatia furaha zaidi. Wakati fulani utaweza kutumia fursa hiyo kumfanya kuwa mwenye furaha.
Kwa mfano, mimi ninapenda sana mkoa wa Kigoma… Sio tu kwa sababu ni kwetu, lakini kwa sababu kuna mambo mengi yenye kuijaza kumbukumbu ya maisha yangu kiasi kwamba huhisi ombwe nisipoyaona mambo hayo.


4.   VIWANGO VYA MAISHA YAKE
Jitahidi sana kujua “living standard” yake kabla ya kuingia katika ndoa. Hilo litakusaidia kujua aina ya mtu unayeingia naye kwenye ndoa na jinsi ya kuamiliana na hali zenu za kiuchumi.

5.   MAISHA YA UTOTONI
Jinsi alivyokua kuanzia utotoni mpaka ukubwa inaweza kuonesha ni mtu wa aina gani. Kujua historia yake, hata yale mambo unayohisi kuwa ni ya kijinga, itakusaidia kumjua mtu wako kwa undani zani.

6.   MIPANGO YAKE KUHUSU FAMILIA
Hili ni jambo muhimu sana kulijua. Naam, alikwambia kuwa anataraji kuwa na familia, lakini alikueleza anahitaji familia ya aina gani? Muulize baadhi ya maswali kuhusu anachokitaka katika familia, na kisha angalia kama yanaendana na matarajio yako.

7.   VIPAJI VYAKE VISIVYOONEKANA
Kuvijua vipawa na vipaji vyake inaweza kukuonesha upande muhimu sana wa mchumba wako. Wanaume wanapenda heshima na upendo, na iwapo utamsifu kuhusu kitu anachokimudu vizuri, atakupenda zaidi ya anavyokupenda sasa.
8.   HISIA ZAKE KUHUSU MAPENZI, NDOA NA TENDO LA NDOA
Hisia zake kuhusu hili zinaweza kuathiri sehemu yote ya ndoa yenu. Huwenda hapendi kubembelezwa anapotoka kazini. Huwenda anapenda shughuli zake kuliko ndoa yenu. Je, nyote mna matarajio ya aina moja kuhusu ukaribu wa kimahabba? Jaribu kujua hisia zake kuhusu upendo, ndoa na tendo la ndoa, na utaweza kujua mengi kuhusu namna uhusiano wako utakavyokuwa huko mbele.

9.   ORODHA YA MAPENDELEO YAKE
Kujua mambo anayoyapenda inaweza kukusaidia sana. Ni muhimu pia kujua mambo makubwa anayotaka kuyafanya katika maisha yake.

10.    ANACHOKIPENDA ZAIDI KUHUSU WEWE
Hili linaweza lisiwe jambo la kawaida kwako, lakini ikiwa utajua mambo anayoyapenda kwako, unaweza kuendelea kuuwasha moto wa mapenzi ndani ya moyo wake. Kujua kwamba anapenda cheko lako itakufanya ucheke zaidi. Labda kitu anachokipenda kwako ni namna unamvyompenda zaidi, na hilo litakufanya uzidi kumpenda.
Iwapo utayajua mambo haya kumhusu, utaimarisha uhusiano wako na kuwa tayari kwa hatua nyingine.

No comments:

Post a Comment

 
 
Blogger Templates